RivotortoRivotorto (jina la Kiitalia lenye maana ya "Kijito kisichonyoka") ni eneo la bondeni chini ya mji wa Assisi ambalo lilipata umaarufu kutokana na Fransisko wa Asizi na wenzake kuishi huko baada ya kurudi kwa furaha toka Roma walipopata kibali cha Papa Inosenti III. Kwanza walibanana katika kibanda fulani huko Rivotorto, halafu wakahamia Porsyunkula. Mahali penyewe panatusaidia sana kuelewa karama ya Kifransisko: si maisha ya kimonaki yanayohitaji kujitegemea kwa mashamba makubwa na mifugo, wala ya wakaapweke wanaohitaji kuishi mbali na watu, bali ni utawa unaohitaji utulivu na upweke kwa ajili ya sala, lakini pia unadai uhusiano mkubwa na watu wa nje ili kupata riziki na hasa kuwajenga kwa mifano na maneno. Hivyo si kati ya watu, wala si mbali nao (kilomita 2-3). Mchana ndugu walikuwa wakienda mjini kufanya kazi mbalimbali ndogondogo na kuwahimiza watu waishi kwa uadilifu. Muda uliobaki, hasa usiku, ulikuwa kwa ajili ya sala upwekeni. Maelezo mengine kuhusu maisha ya wakati huo tunayapata tena katika wasia ambamo Fransisko ametuachia ukumbusho wa kudumu. Tanbihi
Viungo vya nje
|