Liuli
Liuli ni kata ya Wilaya ya Nyasa katika Mkoa wa Ruvuma, Tanzania. Hadi mwaka 2012 ilikuwa sehemu ya wilaya ya Mbinga. Katika sensa iliyofanyika mwaka 2022 wakazi walihesabika kuwa 15,664 [1]. Kwa mujibu wa sensa iliyofanyika mwaka wa 2012, kata ilikuwa na wakazi wapatao 12,611 waishio humo.[2] Liuli ni kijiji kilichopo kwenye mwambao wa ziwa Nyassa. Inajulikana hasa kutokana hospitali ya St. Anne ya kanisa Anglikana inayohudumia wagonjwa wa eneo kubwa sana. Wakati wa koloni ya Kijerumani Liuli iliitwa "Sphinxhafen" yaani bandari ya sfinksi kwa sababu hapa kuna miamba mikubwa inayofanana na sanamu mashuhuri kwenye piramidi za Giza (Misri). Mapigano ya mwaka 1914Tarehe 13 Agosti 1914, mwanzoni wa Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia, Waingereza walishambulia hapa meli pekee ya Wajerumani kwenye ziwa hili. Uingereza iliwahi kuingia katika vita hii tarehe 4 Agosti 1914. Siku chache baadaye nahodha Mwingereza Edmund Rhoades katika Nkhata Bay (Nyassaland - leo Malawi) alipokea amri ya kushika au kuzamisha meli Hermann von Wissmann iliyokuwa meli ya pekee ya Wajerumani kwenye ziwa hili. Meli hii ilikuwa chini ya nahodha Berndt. Rhoades aliendesha meli yake HMS Gwendolyn kuelekea Sphinxhafen (Liuli) kwa sababu alijua meli ilikuwa wapi. Hali halisi manahodha wote wawili walikuwa marafiki waliowahi kutembeleana mara kwa mara na kukaa pamoja. HMS Gwendolyn ilipokaribia bandari mpiganaji wa mzinga wa pekee la meli - mfanyabiashara mmoja Mskoti aliyekuwa pia mtu wa pekee mwenye kujua matumizi yake- alianza kufyatulia risasi dhidi ya Hermann von Wissmann. Dakika chache baadaye boti ndogi ilikaribia haraka HMS Gwendolyn. Nahodha Berndt akapanda meli na kumwuliza mwenzake kwa hasira kwa nini ameshalewa wakati wa mchana. Hakujua bado ya kwamba vita ilianza tayari katika Ulaya. Rhoades alimwarifu na kumtangaza mfungwa wa vita. Habari ya ushindi huu ulipelekwa London kwa simu na tarehe 16 Agosti gazeti la Times ilitangaza "Naval victory on Lake Nyasa" . Wakati ule Waingereza waliondoa mzinga mdogo wa meli na vipuli kadhaa ili meli isitumike tena bila kuiharibu. Mwaka 1915 Wajerumani walikuwa wameleta tena vipuli na kutengeneza meli na hapo Waingereza walirudi Liuli na kuzamisha Hermann von Wissmann. Baada ya vita meli ilifufushwa tena na kufanya kazi kwa Wiangereza. TanbihiMarejeo
|