Cadimi
Cadimi (pia: Kadimi - kupitia Kilatini "Cadmium" kutoka Kigiriki καδμεία kadmeia iliyotaja mitapo yenye cadimi kwa heshima ya mungu wa Kigiriki Κάδμος Kadmos) ni elementi na metali haba duniani. Kikemia ni elementi ya mpito yenye kifupi cha Cd na namba atomia 48 katika mfumo radidia. Tabia na matumiziCadimi ni metali laini yenye rangi nyeupe-buluu. Hufanana mara nyingi na tabia za zinki lakini humenyuka kwa urahisi zaidi. Cadimi yenyewe na kampaundi zake huwa sumu na kusababisha kansa. Matumizi yake ni hasa katika betri na viungo vya rangi. Kwa teknolojia ya kinyuklia hutumiwa kama kinga dhidi ya nyutroni katika matanuri ya nyuklia. Nondo za Cadimi zilitumiwa na Enrico Fermi mwaka 1942 katika tanuri nyuklia ya kwanza kwa kusudi la kutawala mmenyuko mfulizo wa nyuklia. Nondo hizo zilisukumwa kati ya nondo za urani na kupunguza mwendo wa nyutroni kati ya nondo za urani.
|